Ulaya
Ulaya (asili ya jina ni neno la Kiarabu ولاية, wilaayatun[1]; inaitwa pia Uropa kutoka Kigiriki: "Ευρώπη", jina la mungu jike Europa) ni bara lililoko katika Kaskazini ya Dunia, likipakana na Bahari ya Aktiki upande wa kaskazini, Bahari ya Atlantiki upande wa magharibi, na Bahari ya Mediterania upande wa kusini. Mpaka wake wa mashariki kwa kawaida hufafanuliwa kupitia Milima ya Ural, Mto Ural, Bahari ya Kaspi, Milima ya Kaukazi, na Bahari Nyeusi, ingawa mipaka hii ni ya kijiografia na kihistoria zaidi kuliko ya kisiasa. Kwa eneo la takriban kilomita za mraba milioni 10.18, Ulaya ni bara dogo la pili baada ya Australia lakini lina idadi kubwa ya watu, ikifikia zaidi ya milioni 750, na hivyo kuwa moja ya maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu duniani.
Ulaya ina historia ndefu na imechangia pakubwa katika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, na kitamaduni duniani. Bara hili lina mataifa 44 yanayotambulika kimataifa, yakiwemo mataifa makubwa kama Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza, pamoja na madola madogo kama Vatikani na Liechtenstein. Umoja wa Ulaya (EU) ni moja ya miungano muhimu ya kisiasa na kiuchumi katika bara hili, ukiwa na wanachama 27. Aidha, Ulaya imekuwa kitovu cha mapinduzi mbalimbali, kuanzia Mapinduzi ya Kitaaluma na ya Viwanda hadi maendeleo ya demokrasia ya kisasa, na imeendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya kimataifa.
Ramani





Utawala
Katika karne ya 20, baada ya vita kuu mbili, nchi mbalimbali za Ulaya zilianza kushirikiana kwa njia mbalimbali:
- Baraza la Ulaya lina nchi wanachama 47
- Mkutano wa usalama na ushirikiano katika Ulaya (Marekani na Kanada ni wanachama pia)
- Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 tangu mwaka 2013.
Kanda za Ulaya
Katika orodha inayofuata kanda zinatajwa katika utaratibu wa Umoja wa Mataifa (UN categorisations/map). Lakini utaratibu huo haukubaliki ndani ya Ulaya kwa nchi za Ulaya ya Kati. Wajerumani, Waaustria, Waswisi, Wacheki, Waslovakia na Wapoland hukubaliana ya kwamba wenyewe si Ulaya ya Magharibi wala ya Mashariki ila Ulaya ya Kati. Kuna majadiliano kuhusu mipaka ya kanda hili yasiyokwisha bado, kwa mfano suala la Hungaria au Latvia.
Orodha ya Nchi na Maeneo ya Ulaya
Tanbihi
1. Kanda zinazotajwa (Ulaya ya Kusini – magharibi n.k.) zinafuata utaratibu wa Umoja wa Mataifa UN categorisations/map. Nchi kadhaa zinazotajwa hapo chini zinaweza kuhesabiwa kuwa sehemu ya Ulaya na pia bara nyingine (Asia, Afrika, au Oceania). Hii inategemea na namna ya kugawa kontinenti; pia wakazi wenyewe wanaweza kujielewa tofauti na majirani yao.
2. Urusi ni nchi ya kontinenti mbili za Ulaya ya Mashariki na Asia; namba za wakazi na za eneo zimetasjwa kwa ajili ya sehemu ya Kiulaya pekee.
3–5. Guernsey, Kisiwa cha Man, and Jersey ni maeneo ya kujitegemea chini ya Taji la Ufalme wa Uingereza.
6. Namba za Ureno hazijumlishi Visiwa vya Madeira, ambazo ni sehemu ya Ureno magharibi ya Marokko katika Afrika.
7. Namba za Hispania hazijumlishi Visiwa vya Kanari magharibi ya Marokko katika Afrika, wa maeneo ya Ceuta na Melilla ambayo ni sehemu za Hispania kwenye pwani ya Moroko, Afrika ya Kaskazini.
8. Namba za Ufaransa hazijumlishi maeneo yake yaliyopo Amerika ya Kati au Kusini, Bahari Hindi au Oceania.
9. Uholanzi: Idadi ya wakazi ni ya 2004; Amsterdam ni Mji Mkuu lakini Den Haag ni makao makuuy a serikali.
10. Armenia huhesabiwa mara nyingi kuwa nchi ya kimabara katika Asia ya Magharibi (kufuatana na kanda za UM) na Ulaya ya Mashariki
11. Azerbaijan huhesabiwa mara nyingi kuwa nchi ya kimabara katika Asia ya Magharibi (kufuatana na kanda za UM) na Ulaya ya Mashariki; idadi ya wakazi na eneo zimetajwa za sehemu ya Ulaya pekee.
12. Kupro huhesabiwa mara nyingi kuwa nchi ya kimabara katika Asia ya Magharibi (kufuatana na kanda za UM) na Ulaya ya Kusini; idadi ya wakazi na eneo zimetajwa za sehemu zisozo chini ya Dola ya Kituruki ya Cyprus.
13. Georgia huhesabiwa mara nyingi kuwa nchi ya kimabara katika Asia ya Magharibi (kufuatana na kanda za UM) na Ulaya ya Mashariki; idadi ya wakazi na eneo zimetajwa za sehemu ya Ulaya pekee.
14. Uturuki ni nchi ya kimabara katika Asia ya Magharibi (kufuatana na kanda za UM) na Ulaya ya Kusini; namba zinazotajwa zinahusiana na sehemu ndogo ya Magharibi pakee iliyomo Ulaya hasa jimbo lote la Istanbul.
15. Kazakhstan huhesabiwa mara nyingi kuwa nchi ya kimabara katika Asia ya Magharibi (kufuatana na kanda za UM) na Ulaya ya Mashariki; idadi ya wakazi na eneo zimetajwa za sehemu ya Ulaya pekee.
Tazama pia
Marejeo
- ↑ Hivyo asili ya neno "Ulaya" ni sawa na "wilaya"; Krapf 1882 Swahili-English dictionary anaeleza: ""ULAYA (WALAYA au WILAYA ya) ... mother-country in contradistinction to colonies, foreign possessions or parts"; Sacleux 1939 Dictionnaire Swahili-Francais anataja kama etimolojia ya Ulaya "Ar. Hind. ولاية wilaya, pays etranger" (=nchi ya kigeni); Madan 1903 "Wilaya, n. (1) native land, home, but commonly used of foreigners, and so (2) Europe. Ulaya Uzungu, Europe. U, Hindi, India. Ulaya wa Wareno, Portugal